Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wachunguzi huru wa UM kuzuru Burundi kuhusu haki za binadamu

Wachunguzi huru wa UM kuzuru Burundi kuhusu haki za binadamu

Wataalam huru wa Umoja wa Mataifa walioteuliwa kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Burundi, wataanza ziara yao ya kwanza nchini humo kuanzia kesho Machi mosi hadi tarehe nane Machi.

Wataalam hao watatu ni sehemu ya tume ya uchunguzi huru ya Umoja wa Mataifa kuhusu Burundi, iliyoanzishwa na Baraza la Haki za Binadamu mnamo Disemba 17, 2015 kufanya uchunguzi katika ukiukwaji wa haki za binadamu kwa minajili ya kuzuia uzorotaji zaidi wa hali ya haki za binadamu nchini humo.

Aidha, wanalenga kuisaidia serikali ya Burundi kutimiza wajibu wake kuhusu haki za binadamu, kuhakikisha kuna uwajibikaji haki za binadamu zinapokiukwa, ikiwemo kwa kuwatambua wanaodaiwa kutenda ukiukwaji huo.

Wataalam hao ni Christof Heyns, ambaye anahusika na mauaji holela, Bi Maya Sahli-Fadel, ambaye ni mtaalam wa Muungano wa Afrika, AU, anayehusika na masuala ya wakimbizi, waomba hifadhi na wakimbizi wa ndani, na Pablo de Greiff ambaye ni mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuendeleza ukweli, haki, fidia na kuhakikisha kutorudiwa ukiukwaji.