Wagombea nafasi ya ukatibu mkuu UM kujieleza mbele ya Baraza Kuu

26 Februari 2016

Mchakato wa kupata Katibu Mkuu wa Tisa wa Umoja wa Mataifa unaendelea kushika kasi ambapo hii leo Rais wa Baraza Kuu la umoja huo Mogens Lykettoft ametangaza kufanyika kwa mazungumzo yasiyo rasmi ya kuwasikiliza wagombea kama moja ya njia ya kuweka uwazi katika mchakato huo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani Bwana Lyketofft amesema hadi sasa wamepokea rasmi majina sita ya wagombea ambapo watatu ni wanawake na watatu ni wanaume na kuna tovuti maalum kwa wagombea hao.

Amesema ili kutoa fursa ya uwazi na kusikika kwa umma kwa wagombea wote kabla ya uteuzi na uchaguzi, tarehe 12, 13 na 14 Aprili mwaka huu, Baraza Kuu litakuwa na mazungumzo yasiyo rasmi akisema..

(Mogens-1)

“Yatakuwa ni mazungumzo ya uwazi, yasiyo rasmi , kwa kuzingatia kuwa maslahi yake kwa umma na mashirika yasiyo ya kiraia. Na tutaomba wagombea kuwasilisha mapema tamko lenye maneno yasiyozidi 2000 kuhusu dira yao. Wagombea watapatiwa dakika 10 za kujieleza kabla ya maswali na majibu. Andiko hilo litawasilishwa mapema kwa wajumbe wa baraza.

image

Bwana Lykettoft akaulizwa iwapo mgombea kutoka ukanda wowote zaidi ya Ulaya Mashariki anaweza kuwasilisha jina lake akasema hakuna kanuni lakini kuna hoja kutoka baadhi ya wajumbe kuwa….(Mogens-2)

“Wanahoji mzunguko wa kikanda kwa maelezo kuwa hadi sasa ukanda wa Ulaya Mashariki ndio pekee kati ya makundi matano ambayo hayajawahi kuwa na Katibu Mkuu. Hakuna pia kanuni kuhusu jinsia lakini tunafahamu kuwa kuna kundi lenye ushawishi kutoka makundi yote matano likishawishi kuwa sasa iwe fursa ya kupata kwa mara ya kwanza Katibu Mkuu mwanamke.

Waandishi wa habari wakataka kufahamu nafasi ya Baraza la Usalama na Baraza Kuu katika uteuzi huo wakionyesha wasiwasi wao kuwa Baraza la Usalama linaweza kutumia kura turufu..

(Mogens-3)

"Kanuni ni rahisi sana na fupi ya kwamba ni uchaguzi unaofanywa na Baraza Kuu baada ya pendekezo lililowasilishwa na Baraza la Usalama. Hicho ndiyo kitu tumeandika na ndio maana Baraza Kuu limetaka kuwa na mazugumzo yasiyo rasmi hata kabla Baraza la Usalama halijaanza mchakato wake. Lakini ni kweli ni hiari ya Baraza laUsalama kuleta jina moja au jina zaidi ya moja lakini mwisho wa siku Baraza Kuu ndio linapiga kura.

Ijapokuwa hakuna ukomo ya idadi ya awamu za kuwa Katibu Mkuu kwa kipindi cha miaka mitano mitano, hadi sasa hakuna Katibu Mkuu ambaye amewahi kuongoza kwa vipindi zaidi ya viwili tangu Katibu Mkuu wa kwanza Trygve Lie wa Norway mwaka 1946.

Katibu Mkuu mpya atafahamika Januari 2017.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud