Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtaalam wa UM kuzuru CAR kufuatilia hali ya haki za binadamu

Mtaalam wa UM kuzuru CAR kufuatilia hali ya haki za binadamu

Mtaalam huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Marie-Thérèse Keita Bocoum, atafanya ziara nchini humo kuanzia Machi mosi hadi Machi 10, 2016, ili kutathmini hali ya sasa ya haki za binadamu, siku chache baada ya duru ya pili ya uchaguzi wa rais.Taarifa kamili na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Akiwapongeza raia wa CAR kwa kushiriki uchaguzi huo kwa amani, na mgombea Faustin Archange Touadéra kwa ushindi wake kwa mujibu wa matokeo ya awali, Bi Keita Bocoum amesema anatumai hatua hiyo muhimu katika kuimarisha demokrasia itachochea kuchukua hatua madhubuti za kufikia amani na utawala wa sheria.

Mtaalam huyo wa haki za binadamu amesema atatumia fursa ya ziara yake kuzungumza na viongozi wa nchi hiyo, kuwafahamisha kuhusu mapendekezo aliyofanya katika ripoti yake iliyopita, na kuwahamasisha watekeleze mapendekezo hayo na ahadi zilizowekwa katika kongamano la kitaifa la Bangui.

Aidha, atakutana na wakuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa CAR, MINUSCA na mabalozi wa nchi husika ili kupata taarifa kuhusu hatua zilizochukuliwa katika kupambana na unyanyasaji wa kingono, au kuwafungulia mashtaka walinda amani waliotekeleza unyanyasaji huo dhidi ya watoto na wanawake, pamoja na hatua za kuwalinda raia.