Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC unyanyasaji dhidi ya vikundi vya kiraia watia hofu OHCHR

DRC unyanyasaji dhidi ya vikundi vya kiraia watia hofu OHCHR

Mashirika ya kiraia huko jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC vimeendelea kukumbwa na manyanyaso wakati huu ambapo fursa ya demokrasia imezidi kutwama nchini humo. Taarifa kamili na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Hiyo ni kwa mujibu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja w a Mataifa OHCHR ikisema kuwa hilo ni dhahiri kwa kuwa wafuasi sita wa kikundi cha kiraia LUCHA wamehukumiwa kifungo cha miaka miwil jela na mahakama ya wilaya ya Goma, Mashariki mwa nchi.

Wafuasi hao sita walikamatwa tarehe 16 mwezi huu kwa madai ya kuchochea mapinduzi dhidi ya serikali wakati maandalizi ya kumbukizi ya mauaji ya waandamanaji jijijini Kinshasa mwaka 1992.

Cecil Pouly ni msemaji wa ofisi hiyo mjini Geneva, Uswisi.

“Tuna hofu pia na kuendelea kushikilwa kwa mfuasi wa LUCHA, Fred Bauma, na mtaalamu wa mitandao Yves Makwambala. Wote hao walikamatwa na maafisa wa serikali wakati wa mkutano wa vijana Kinshasa na wanakabiliwa na mashtaka ya kutishia usalama wa nchi. Kumekuwepo na madai ya watu kukamatwa na kushikiliwa kiholela, ukiukwaji wa haki na kushindwa kupata msaada wa kisheria, kadhalika kutia saini taarifa bila kufahamu kilichomo.”

Kwa mujibu wa ofisi hiyo polisi na maafisa wa usalama walitia korokoroni watu 45 huko Kinshasa, Goma, Uvira na Lubumbashi wakati wa siku ya kumbukizi ya mauaji hayo ambapo walengwa walikuwa wanachama wa vyama vya upinzani na mashirika ya kiraia.