Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua zaidi zahitajika kufikisha misaada kwa wahitaji huko Syria - de Mistura

Hatua zaidi zahitajika kufikisha misaada kwa wahitaji huko Syria - de Mistura

Nchini Syria kumekuwepo na mafanikio katika kufikishia misaada wahitaji hasa kwenye maeneo yaliyozingirwa, lakini hatua zaidi zahitajika.

Amesema mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, Staffan de Mistura huko Geneva, Uswisi alipozungumza na waandishi wa habari wakati huu ambapo kuna walakini juu ya usitishwaji wa chuki baina ya pande kinzani.

De Mistura ambaye alizungumza baada ya kikao cha kikosi kazi kwa usaidizi wa Syria, amesema karibu malori 200 yenye shehena za misaada sambamba na misaada iliyoangushwa kutoka angani imefikishwa kwa wahitaji katika siku za karibuni.

Hata hivyo amesema duniani inatazama iwapo wapiganaji huko Syria wataweka chini silaha zao ifikapo Ijumaa usiku, ambapo ni siku ya mwisho ya kuwa wametekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano.

“Hakuna kinachotosheleza. Hatua zaidi zahitajika na watu wengi zaidi wanahitaji kufikiwa ili wapate misaada. Na iwapo, kama tunavyotumai usitishaji mapigano utazingatiwa kama tulivyotumai, hiyo itakuwa na manufaa kwenye kufikia wahitaji huko Syria, siyo tu kwenye maeneo yaliyozingirwa, bali kote kwingineko nchini humo.”

Amesema iwapo usitishaji mapigano utafanikiwa, basi itakuwa ni fursa kwa kuanza tena kwa mazungumzo kwa ajili ya Syria ambayo yalikuwa yamesitishwa.

Kwa upande wake, mwenyekiti mwenza wa ISSG Jan Egeland amesifu hatua iliyofikiwa akisema wanahaha kuhakikisha wanawasiliana na vikundi vinavyopigana ikiwemo serikali ili kuwezesha misaada kufika.

Zaidi ya watu 480,000 bado wanahitaji misaada kwenye maeneo 17 yaliyozingira nchini Syria.