Skip to main content

Marais watano wa Afrika watua Burundi kusaka suluhu

Marais watano wa Afrika watua Burundi kusaka suluhu

Ujumbe wa Marais watano wa Afrika umewasili Burundi hii leo katika  jitihada za  kujaribu  kutanzua mgogoro wa kisiasa nchini humo uliodumu zaidi ya miezi kumi  na kushuhudia mauaji  ya watu zaidi 400 huku zaidi ya  raia laki mbili unusu wakilazimika kutoroka  nchi na  kuchukua  hifadhi katika chi jirani. Katibu Mkuu wa Umoja wa  Mataifa Ban Ki Moon alikuwa Burundi wiki hii na kuhakikishiwa na serikali  azma yake ya kuanzisha mazungumzo jumuishi. Kutoka bujumbura, mwandishi wetu Ramadhani KIBUGA anasimulia zaidi.

(Taarifa ya Kibuga)

Rais wa Afrika ya Kusini Jacob Zouma  ndiye anaongoza ujumbe huo akiwa na Marais  Macky Sall wa Senegal, wa Mouritania Mohamed Ould Abldel Azzi, Rais wa Gabon Ali Bongo Ondimba na waziri Mkuu wa Ethiopia  Haile mariam  Desalegn.

Kulingana na ratiba ,  viongozi hao wa Afrika watakutana na wadau mbali wa siasa za Burundi ikiwa ni pamoja na wakuu wa vyama vya kisiasa, wawakilishi wa asasi za kiraia,  wakuu wa dini na madhehebu  kabla ya kuwa na mazungumzo na Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza.

Awali  Muungano wa Afrika uliazimia  kutuma vikosi  5000 vya  vya walindamani   nchini humu ,  lakini kutokana na upinzani mkali wa serikali ya Burundi,   AU ikaachana na mpango huo.

Kwa sasa Marais hao watakuwa  na shughuli ya kuishawishi  serikali  kuketi meza moja na upinzani na kufufua mazungumzo jumuishi ambayo yalikwama tangu mwezi disemba  licha ya kuzinduliwa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda mwezi disemba mwaka jana baada ya serikali kupinga kujadiliana na sehemu moja  ya wapinzani kwa madai kwamba wamesimamia vurugu nchini.

Waziri wa mambo ya nje wa Afrika Kusini  Maite Nkoana Mashabane  ameelezea matumaini makubwa.

“ Tuko hapa Kuunga mkono Rais Zuma na marais wengine wanne wanaounda Ujumbe huu wa ngazi ya juu kuweka msukumo mchakato wa amani unaoendelea. Tangu tulipofika tumeona kwamba kuna hatua fulani iliofikiwa na kwamba kuna utashi wa kuendeleza mchakato huu. Ujumbe tumekuja nao ni ujumbe wa amani.Tunaunga mkono kile chote kinacholeta amani na usalama, lakini  kwa kuzingatia nini warundi wenyewe wanahitaji kama uungwaji mkono.