Makubaliano ya polisi Ulaya yaweka wakimbizi hatarini: Zeid

25 Februari 2016

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa Zeid Ra' ad Al Hussein ameelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu harakati za kiusalama zilizochukuliwa na wakuu wa polisi wa nchi tano za ulaya, akisema zitakuwa na madhara mabaya kwa haki za binadamu za wakimbizi na wahamiaji kwenye ukanda wa Ulaya mashariki na Kusini.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo Kamishna Zeid amesema  tayari baadhi ya wakimbizi na wahamiaji wameanza kufukuzwa kwenye njia inayopitia Austria, Slovenia, Croatia, Serbia na Macedonia.

Ameongeza kuwa kufuatia hatua hiyo mamia ya Waafghan wamezuiwa na kufungwa kwenye eneo la mpakani kati ya Serbia na Macedonia kwa msingi wa uraia wao.

Kamishna Zeid amesema kwamba anaelewa changamoto zinazozikumba mamlaka za serikali za baadhi ya nchi za Ulaya zikikabiliwa na wimbi la wahamiaji, hata hivyo amesema harakati zilizochukuliwa zinakiuka sheria ya kimataifa.

Amezisihi nchi za Ulaya kuchukua hatua ili kupambana na ubaguzi na fikra potofu kuhusu wahamiaji ambazo zimezuia jitihada za seikali kutunza haki za kundi hilo.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter