Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti ya UM yaorodhesha ukiukwaji mkubwa na unyanyasaji Libya:

Ripoti ya UM yaorodhesha ukiukwaji mkubwa na unyanyasaji Libya:

Ripoti ya Umoja wa mataifa iliyochapishwa Alhamisi imeorodhesha kutapakaa kwa ukiukwaji mkubwa na unyanyasaji uliotekelezwa nchini Libya tangu mwanzo wa mwaka 2014.

Ripoti inapendekeza hatua za haraka za kukomesha ukwepaji wa sheria, kuimarisha na kufanyia marekebisho sekta ya sheria nchini humo.

Kwa mujibu wa kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein, licha ya hali ya haki za binadamu nchini Libya ni nadra kugonga sana vichwa vya habari, lakini watendaji wengi , wa serikali na wasio wa serikali wanatuhumiwa kwa ukiukwaji mkubwa sana na dhuluma ambayo inaweza, katika visa vingi kuwa uhalifu wa kivita.

Miongoni mwa ukiukaji huo na unyanyasaji ni mauaji ya kinyume cha sheria, mashambulizi ya kiholela, mateso na shuluba, watu kutiwa kizuizini kiholela, utekaji na watu kutoweka, ukatili wa kijinsia na ubaguzi dhidi ya wanawake.

Miongini mwa waathirika wakubwa ni pamoja na waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu, wahamiaji, watoto na wanawake.

Ripoti imetoa wito wa jumuiya ya kimataifa kuhakikisha kwamba mahakama ya kimataifa ya uhalifu ambayo ina mamlaka dhidi ya Libya , kuwa na rasilimali za kutosha kufanya uchunguzi wake na kuhukumu kuwafungulia mashitaka wahusika.