Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Akiwa DRC, Ban akutana na Kabila, ahimiza ushirikiano na MONUSCO

Akiwa DRC, Ban akutana na Kabila, ahimiza ushirikiano na MONUSCO

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ambaye yuko ziarani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DCR, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo.

Taarifa ya msemaji wake imesema kuwa, wakati wa mkutano wao, Katibu Mkuu amehimiza serikali ya DRC kuendelea kufanya mazungumzo ya kimkakati na ujume wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO, pamoja na kubuni mkakati wa kuondoka kwa ujumbe huo nchini DRC.

Kwa mantiki hiyo, amekaribisha tangazo la kurejelewa kwa ushirikiano kati ya jeshi la DRC, FARDC na MONUSCO, kama hatua muhimu katika kuboresha ulinzi wa raia, kupunguza tishio linalotokana na kuwepo vikundi vyenye silaha, na kuimarisha hali mashariki mwa DRC.

Aidha, Ban amezungumzia ziara yake hapo jana kwa kambi ya wakimbizi wa ndani ya Kitchanga, Kivu Kaskazini, kama mfano wa changamoto za kibinadamu zinazoikabili dunia, na kumualika Rais Kabila kuhudhuria mkutano wa viongozi wa dunia kuhusu masuala ya kibinadamu mwezi Mei mwaka huu, 2016, mjini Istanbul, Uturuki.