Sudan Kusini yazindua ripoti ya kwanza ya maendeleo ya binadamu

Sudan Kusini yazindua ripoti ya kwanza ya maendeleo ya binadamu

Serikali ya Sudan Kusini na shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP wamezindua ripoti ya kwanza kabisa ya hali ya maendeleo ya kibinadamu nchini humo.

Ripoti hiyo imezinduliwa wakati taifa hilo changa zaidi duniani likikabiliwa na changamoto za kiuchumi, kisiasa na kijamii huku likihaha kusaka mbinu za kujikwamua.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo yenye maudhui, Watu, Amani na Ustawi Naibu Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa MAtaifa Sudan Kusini Eugene Owusu amesema..

(Sauti ya Eugene)

“Sudan Kusini inaweza kufikia mustakhabali itakayo. Hali ambayo Sudan Kusini inakabiliana nayo hii leo ni mchanganyiko wa vitendo vya binadamu ambavyo vinaweza kusahihishwa iwapo wasudan Kusini wenyewe wataipatia fursa amani. Kukiwepo na mseto bora wa sera, na hali ya kuwa na malengo na azma ya kile kilichochea uhuru wa nchi hii, Sudan Kusini inaweza ikajikwamua kwenye changamoto inazokumbana nazo leo hii.”

Kwa upande wake Makamu Rais wa Sudan Kusini Wani Igga ametoa wito kwa wananchi kushiriki kwenye shughuli zenye tija akiongeza kuwa uhuru wa nchi hiyo utakuwa hauna maana iwapo hakuna amani  na maendeleo.

Ripoti hiyo pamoja na mambo mengine inaweka mahitaji na mwelekeo wa kuwezesha Sudan Kusini kustawi.