Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNHCR aeeleza wasiwasi kuhusu kufungwa kwa mipaka ya Ulaya

Mkuu wa UNHCR aeeleza wasiwasi kuhusu kufungwa kwa mipaka ya Ulaya

Ulaya inachochea mzozo mkubwa zaidi wa wakimbizi ikiongeza vikwazo mipakani mwake.

Huu ni ujumbe wa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Wakimbizi, Filippo Grandi, akiwa ziarani Ugiriki kwenye kisiwa cha Lesvos ambako huwasili maelfu ya wakimbizi kila siku kutoka Uturuki.

(Sauti ya Bwana Grandi)

“Nina wasiwasi mkubwa kuhusu taarifa tunazopata za kufungwa zaidi kwa mipaka ya Ulaya kwenye njia za kupitia Balkans, Ulaya Mashariki. Hii ni kwa sababu itasababisha vurugu zaidi na mkanganyiko na itazidisha mzigo kwa Ugiriki ambayo tayari inakumbwa na wajibu mkubwa wa kushughulikia watu hawa.”

Hata hivyo Bwana Grandi amepongeza askari wa Ugiriki kwa jitihada zao katika kuokoa wakimbizi wanaopata shida wakati wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterenia.

Mwaka jana, watu wapatao 500,000 wamekimbilia Ulaya kupitia kisiwa cha Lesvos ambapo Bwana Grandi amesisitiza umuhimu kwa nchi wanachama wa Ulaya kujitolea zaidi ili kuwapatia wakimbizi hao makazi na huduma mbali mbali.

Amesikitishwa pia na ubaguzi dhidi ya wakimbizi kwa msingi wa uraia wao ambapo waSyria na waIraqi wanakubaliwa ilhali waSomali, waAfghan na wapalestina wanazuiwa.