Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vunjeni mzunguko wa ukimya na kukubali ukatili dhidi ya wanawake:UM

Vunjeni mzunguko wa ukimya na kukubali ukatili dhidi ya wanawake:UM

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa mataifa kuhusu ukatili dhidi ya wanawake, sababu na athari zake Dubravka Šimonović leo amekaribisha maendeleo muhimu katika sheria za Georgia kuhusu usawa wa kijinsia na ukatikli dhidi ya wanawake, lakini ameonya kwamba mabadiliko makubwa zaidi yanahitajika katika mtazamo wa jamii dhidi ya ukatili wa kijinsia ikiwemo unyanyasaji majumbani na ndoa za mapema.

Bi Šimonović amesema kuna haja ya haraka kuvunja mzunguko wa ukimya na kukubali ukatili dhidi ya wanawake kama masuala binafsi na kuhakikisha haki ya kila mwanamke na msichana ya kuishi maisha huru bila ukatili.

Ameyasema hayo katika mwisho wa ziara yake ya kwanza nchini Georgia, akiongeza anatambua kupitisha hivi karibuni sheria mpya za usawa wa kijinsia, kutokubagua na ukatili majumbani , ili kuhakikisha zinaenda sanjari na viwango vya kikanda na kimataifa nchini humo.

Ametoa wito wa kuridhia haraka mkataba wa Instanbul, ambao ni muafaka wa Ulaya wa kushughulikia ukatili dhidi ya wanawake na unyanyasaji majumbani. Pia amependekeza kuundwa kwa vituo maalumu vya serikali kwa ajili ya kuwahifadhi wanawake na wasichana walioathirika na ukatili wa kijinsia. Baada ya siku tano za ziara Georgia atawasilisha ripoti na mapendekezo kwenye baraza la haki za binadamu mwezi Juni mwaka huu.