Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu wa Syria wanahitaji kuona tofauti katika hali yao sasa- O’Brien

Watu wa Syria wanahitaji kuona tofauti katika hali yao sasa- O’Brien

Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu Katika Umoja wa Mataifa, Stephen O’Brien, ameliambia Baraza la Usalama la Umoja huo kuwa mzozo wa Syria hauwezi kutatuliwa iwapo hali ya kutowalinda kabisa raia nchini humo itaendelea.

Akikumbusha kuwa watu wa Syria wameteseka kwa muda mrefu, na kwamba mzozo huo utakuwa umedumu kwa miaka mitano mwezi ujao, Bwana O’Brien amesema jamii ya kimataifa imekuwa ikitizama tu, huku mzozo huo wa Syria ukizidi kuwa mkubwa zaidi na wenye uharibifu mkubwa zaidi katika kizazi cha sasa

“Watu wa Syria ambao sasa hawaamini iwapo jamii ya kimataifa ina hamu ya kumaliza vita nchini mwao baada ya miaka ya kutochukua hatua, wanahitaji kuona tofauti katika maisha yao mara moja, kwani hadi sasa, ni wao ndio wanaotaabika kwa madhara ya mzozo huu, kwa sababu ukatili umekuwa ulioenea, wa kupangwa na uliokithiri.”

O’Brien amekaribisha tangazo lilitolewa na Marekani na Urusi la makubaliano ya kusitisha mapigano kote nchini Syria, ambayo yamepangwa kuanza kutekelezwa mwishoni mwa wiki hii. Amesema tangazo hilo ni ishara iliyosubiriwa kwa muda mrefu na watu wa Syria

“Ni vigumu kuamini kuwa mzozo huu unaweza kutatuliwa iwapo raia wataendelea kutolindwa kabisa. Makubaliano ya kusitisha uhasama ni lazima hatimaye yazalishe kile ambacho hakikuweza kuzalishwa na maazimio ya Baraza hili na kanuni za msingi za sheria ya kimataifa: yaani kukomeshwa mara moja mashambulizi holela dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia, na kuimarishwa ulinzi wa raia. Na itoshe! Ukatili huu ni lazime ukomeshwe.”

Halikadhalika, O’Brien amesema kuwazingira na kuwalazimishia raia njaa kama mbinu ya vita ni lazima kukomeshwe mara moja, akikumbusha kuwa wajibu wa kutekeleza hilo ni wa pande zinazofanya hivyo, na wale wanaowaweka raia hatarini kwa kuwatumia kama ngao za vitendo vya kijeshi katika maeneo yaliyozingirwa.