Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNDP yaadhimisha miaka 50 kwa kuwa na ufanisi zaidi

UNDP yaadhimisha miaka 50 kwa kuwa na ufanisi zaidi

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo UNDP linaadhimisha leo miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, likiwa sasa linafanya kazi kwenye nchi 170 duniani kote miongoni mwao 46 zikwa barani Afrika.

Akihutubia mkutano wa mawaziri uliofanyika leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuadhimisha siku hiyo, mkuu wa UNDP Helen Clark amemulika umuhimu wa ubia na nchi wanachama ili kuwawezesha kukuza maendeleo kwa ngazi ya kitaifa, akieleza jinsi UNDP imejitahidi kubadilika ili kuimarisha ufanisi wake

(Sauti ya Bi Clark)

"Tuna na mpango madhubuti, tumebadilisha shirika letu ikiwemo kupeleka sera zetu na miradi yetu karibu zaidi na nchi kwenye maeneo husika. Tumechukua hatua hadi UNDP imeorodheshwa kama moja ya mashirika ya maendeleo yenye uwazi zaidi duniani. Hata hivyo tunajua kwamba tunapaswa kuweza kuitikia kwa kasi zaidi na kuwa wabunifu zaidi."

Bi Clark amesema lengo la mkutano huo wa mawaziri ni kubuni mikakati ya maendeleo ya kitaifa inayoweza kusaidiwa na UNDP.

Kwa upande wa Tanzania, UNDP imeanza operesheni zake mwaka 1978 ikiwa sasa hivi inatekeleza miradi ya kutunza misitu, kukuza vyanzo mbadala vya nishati, kuendeleza utawala bora Zanzibar na bara, na kusaidia serikali kupambana na janga la ukimwi.