Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushiriki wa jamii katika usimamizi wa misitu waleta nuru- Ripoti

Ushiriki wa jamii katika usimamizi wa misitu waleta nuru- Ripoti

Ripoti mpya ya Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), imesema, juhudi za kijamii za upanzi na uhifadhi wa misitu, zinaweza kusaidia kuimarisha maisha endelevu ya mwanadamu. Taarifa kamili na John Kibego.

(Taarifa ya Kibego)

Kwa mujibu wa ripoti hiyo illiyotolewa leo, kwenye ufunguzi wa wiki ya Misitu katika ukanda wa Asia Pasifiki, ushiriki wa jamii katika usimamizi wa mistu umetoa matumaini makubwa ingawa bado fursa hiyo haijatumiwa vipasavyo.

Chini ya usimamizi huu, wenyeji hushirikiana na serikali katika kuamua jinsi ya kutumia ardhi na usimamizi wa rasilimali za misitu ambazo ni tegemeo kwa maisha.

FAO inataja harakati zinazohitajika kupata matunda zaidi kutokana na juhudi hizo kuwa ni pamoja na kuhakikisha usalama katika umiliki wa misitu, kupata muongozo wa kisheria na kusambaza ujuzi na teknologia sahihi na nafuu kwa jamii hizo.

Dominique Reeb ni Afisa kutoka FAO, kitengo cha masuala ya misitu.

(Sauti ya Dominique)

" Tumeshuhudia kwamba wakati watu wasipokuwa na haki za umiliki rasilimali , kwa kawaida wanaiharibu au kushusha thamani ya rasilimali hizo kwa sababu hawaizmiliki, lakini mara unapowakabidhi jamii haki ya rasilimali hizo basi wadau hawa wanaithamini na kuitunza kwa kiasi kikubwa sana"

Ripoti imeongezea kuwa, ni muhimu kuimarisha ujuzi wa jamii hizo na wamiliki wadogo wadogo wa misitu kuhusu masuala ya masoko ya bidha za misitu, jambo ambalo linaweza kuchangia kiasi kikubwa kupunguza umaskini.