Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waziri wa fedha wa Rwanda asema ushirikiano zaidi wahitajika kwenye mfumo wa UM

Waziri wa fedha wa Rwanda asema ushirikiano zaidi wahitajika kwenye mfumo wa UM

Leo Baraza la Umoja wa Mataifa la Kiuchumi na Kijamii limekutana kujadili operesheni za Baraza hilo kwa mwaka 2016, likiangazia hasa utekelezaji wa ajenda ya mwaka 2030.

Akihutubia kikao hicho Rais wa Baraza Kuu Mogens Lukketoft amesema ni wajibu wa nchi wanachama kutamka wanachohitaji kutoka kwa Umoja wa Mataifa ili muundo huo uwasaidie katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu.

Waziri wa Fedha wa Rwanda Claver Gatete akatoa mapendekezo kuhusu jinsi ya kuimarisha ufanisi wa Umoja wa Mataifa wakati ambapo ukuaji wa uchumi unapungua duniani kote na hivyo ufadhili wa maendeleo unakuwa finyu zaidi.

(Sauti ya Waziri Gatete)

“ Mabadiliko mengi yanatekelezwa ili kuimarisha kazi ya mfumo wa Umoja wa Mataifa kwa ngazi ya kitaifa kupitia utaratibu wa Delivery As One. Lakini hatujashuhudia kiasi hicho cha uwazi na ushirikiano kwa ngazi ya kikanda na kimataifa. Tathmini thabiti inahitajika ili kubuni maeneo mapya ambapo Mfumo wa Umoja wa Mataifa unaweza kuimarisha ufanisi wake na kuleta mabadiliko, yakiwemo ukusanyaji ufadhili, nguvu za watu, kujenga utalaam na ujuuzi kuhusu maswala ya utapiamlo, athari za majanga, mabadiliko ya tabianchi, amani na usalama.”

Bwana Gatete ameeleza kwamba mafanikio ya Rwanda katika maendeleo yamesababishwa na ubunifu, uwajibikaji wa serikali, uongozi wenye dira, na taasisi imara zinazoendeshwa kwa kulenga matokeo, ambayo yamesaidiwa na mfumo wa Umoja wa Mataifa, ulioanzisha utaratibu wa kufanya kazi kwa pamoja nchini humo kupitia utaratibu wa Delivery As One.