Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akaribisha muafaka uliotangazwa leo wa usitishaji mapigano nchi nzima Syria

Ban akaribisha muafaka uliotangazwa leo wa usitishaji mapigano nchi nzima Syria

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon amekaribisha tangazo la muafaka wa usitishaji mapigano Syria, lililotolewa leo na waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergey Lavrov,kama wenyeviti wa kundi la kimataifa la msaada kwa Syria ISSG katika kusitisha mapigano lililoundwa Munich.

Muafaka huo wa usitijshaji mapigano unatarajiwa kuanza kutekelezwa nchi nzima Ijumaa Februari 27 mwaka huu wa 2016 ..

Akitambua muda na mjadala uliopepekea hatua hii Ban amesema anaamini makubaliano, kama yataheshimiwa itakuwa hatua muhimu katika kuelekea utekelezaji wa azimio la baraza la usalama nambari 2254(2015).

Amesema inaonyesha nia ya ISSG kwa kutumia ushawishi kwa pande zinazopigana ili kupunguza haraka vurugu kama hatua ya kwanza kuelekea usitishaji mapigano wa muda mrefu. Pia inachangia kujenga mazingira mazuri kwa ajili ya kuanza upya kwa mazungumzo ya kisiasa. Zaidi ya yote, ni ishara ya matumaini iliyosubiriwa kwa muda mrefu kwa watu wa Syria kwamba baada ya miaka mitano ya vita kunaweza kuwa na mwisho wa mateso .

Ban amezitaka pande zote kuzingatia matakwa ya muafaka, na kusema kazi kubwa sasa ni kuhakikisha utekelezaji na jumuiya ya kimataifa, ISSG na pande kinzani lazima zisimame imara katika maamuzi yao.