Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni wajibu wa kila nchi kulinda vifaa nyuklia dhidi ya magaidi- IAEA

Ni wajibu wa kila nchi kulinda vifaa nyuklia dhidi ya magaidi- IAEA

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), Yukiya Amano, amasema kuna haja ya nchi zote kuweka sheria zinazofanya usafirishaji wa vifaa vya nyuklia kuwa kosa la jinai, pamoja na kuchukua hatua zifaazo za kuzuia na kukabiliana nao.

Akiongea wakati wa mkutano kuhusu mkataba kuhusu ulinzi wa nyuklia, Bwana Amano amesema kwamba, wasafirishaji haramu wa vifaa vya nyuklia wanaweza kutafuta njia ya kuvivushia nchi yoyote duniani, hususan kwa kulenga udhaifu katika mitandao ya kiusalama.

Aidha, Amano amesema kuanza kutekelezwa kwa marekebisho ya mkataba kuhusu ulinzi wa vifaa vya nyuklia kutapunguza uwezekano wa magaidi kuweza kulipua bomu la kusambaza mionzi ya nyuklia.

Mkuu huyo wa IAEA amesema kuwa usalama wa vifaa vya nyuklia siyo tu wajibu wa nchi zenye mipango ya nishati ya nyuklia, lakini unahitaji uratibu wa kimataifa, kwani hatari zitokanazo na kutokuwepo usalama wa nyuklia zinavuka mipaka.