Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahisani timizeni ahadi zenu kwa wananchi wa Libya - UM

Wahisani timizeni ahadi zenu kwa wananchi wa Libya - UM

Hali ya kibinadamu nchini Libya inazidi kuzorota na  usaidizi wa haraka unahitajika, amesema Naibu mwakilishi wa katibu Mkuu wa Umoja  wa Mataifa nchini humo Ali Za’atari.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Cairo, Misri, Bwana Za’tari amesema wanahitaji misaada yenye thamani ya dola Milioni 166 ili kusaidia watu Milioni 2.4.

Amesema hadi sasa wamepata asilimia 2.6 tu ya mahitaji yote, akisema kusuasua kwa misaada kunahatarisha mustakhbali wa raia.

Bwana Za’atari amesema wao hawana shida kuwafikia walengwa kwa ajili ya kuwapatia misaada, ila tatizo ni jamii ya kimataifa kutotekeleza ahadi ya fedha ili kuweza kununua vifaa tiba, chakula, maji na huduma nyingine muhimu.

Akiwa Misri, atakuwa na mkutano na viongozi wa nchi hiyo na wale wa Umoja wa nchi za kiarabu ili kuelezea hali halisi ya janga la kibinadamu Libya.