Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Ki-moon awasili Burundi katika harakati za kusaka usuluhishi

Ban Ki-moon awasili Burundi katika harakati za kusaka usuluhishi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amewasili jioni hii mjini Bujumbura, Burundi katika juhudi za kujaribu kukwamua mzozo wa kisiasa uliodumu kwa zaidi ya miezi kumi nchini humo kufuatia muhula wa tatu wa rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza. Kwenye Uwanja wa ndege wa Bujumbura amelakiwa na Makamu wa Kwanza wa Rais Gaston Sindimwo akiwa pamoja na waziri wa mambo ya nje Alain Aime Nyamitwe. Kutoka Bujumbura, mwandishi wetu Ramadhani Kibuga anatuarifu zaidi.

(Taarifa ya Kibuga)

Bwana Ban Ki-moon amewasili kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bujumbura saa 11 jioni.

Kulingana na ratiba, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atakuwa na mazungumzo jioni hii ya jumatatu na wakuu wa vyama vya siasa , lakini vile vile Mashirika yasiokuwa ya serikali yanayohudumu Burundi kabla ya kukutana kwa mazungumzo na waziri wa mambo ya nje Alain Nyamitwe

Aidha kulingana daima na ratiba hiyo Bwana Ban Ki-moon atakuwa na mazungumzo ya ana kwa ana na Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza ofisini mwake jumanne asubuhi .

Viongozi hao wawili watakuwa na mazungumzo na vyombo vya habari muda mfupi kabla ya Ban Ki-moon kuendeleza duru yake katika nchi jirani ya DRC na baadae Sudan Kusini.

Ziara ya Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa nchini hapa Burundi inadhamiria kukwamua mgogoro wa kisiasa uliodumu kwa zaidi ya miezi kumi kufuatia muhula wa tatu wa Rais Nkurunziza.

Bwana Ban anataraji kumushawishi Rais wa Burundi kukubali mazungumzo jumuishi na wapinzani lakini vilevile kuzungumzia kuhusu visa vya ukiukwaji wa haki za binaadamu vinayoshuhudiwa nchini tangu mzozo uliporipotiwa.

Katika kile kinachoonekana kama kulegeza misimamo , Serikali ya Burundi imeondoa waranti 15 za kukamatwa Viongozi wa Kisiasa waliokuwa wanasakwa na vyombo vya kimataifa kwa jumla ya wanasiasa 34 wa upinzani. Ni wiki hii pia serikali ya Burundi imeazimia kufungua redio 2 za binafsi na kuwaruhusu wachunguzi 25 wa kimataifa wa haki za binaadamu kutoka Muungano wa Afrika.