Hakuna likizo kwa Wairaq waliochukua hifadhi kwenye hoteli iliyobomoka:UNHCR

Hakuna likizo kwa Wairaq waliochukua hifadhi kwenye hoteli iliyobomoka:UNHCR

Jumba la ghorofa sita ambalo liliwahi kuwa moja ya hotel maarufu za kitalii Iraq na kisha kukumbwa katika mapigano na kutelekezwa na watalii sasa ni maskani ya mamia ya Wairaq wanaokimbia machafuko kwenye jimbo la Anbar.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR jumba hilo la Habbaniyah ambalo sasa limesalia kama gofu likiwa na mabwawa ya kuogelea yasiyo na maji, pia halina umeme wala huduma muhimu za usafi na mfumo wa maji taka.

Takribani familia 400 zinaishi katika jingo hilo ambalo kwa tathimini ya mhandisi wa Iraq liko katika hatari ya kuporomoka. UNHCR inaamini kwamba hoteli hiyo ya zamani si salama na ni hatari kwa afya ya familia zinazoishi hapo hasa kwa mlipuko wa maradhi.

Shirika hilo limesema linajenga malazi mbadala karibu na eneo hilo ambayo yatakamilika baada ya mwezi mmoja.