Matokeo ya uchaguzi CAR yatangazwa, Ban atoa kauli

Matokeo ya uchaguzi CAR yatangazwa, Ban atoa kauli

Matokeo ya awali ya uchaguzi wa Rais nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR yametangazwa huku Faustin Archange Touadéra  akitangazwa kuibuka mshindi dhidi ya mpinzani wake Anicet Dologuele.

Kufuatia kutangazwa kwa matokeo hayo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amempongeza Bwana Touadéra  huku akisifu kitendo cha Dologuele kukubali matokeo hayo kupitia hotuba yake.

Bwana Ban katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake pia amepongeza wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa jinsi walivyoshiriki uchaguzi huo wa tarehe 14 Februari kwa amani.

Halikadhalika ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa na wadau wa kitaifa kuendeleza mazingira stahili na kwa washiriki wote kuzingatia ahadi zao kwa mujibu wa sharia za uchaguzi.

Katibu Mkuu ametoa wito kwa mamlaka za mpito nchini humo kukamilisha mchakato wa uchaguzi kwa kuhakikisha awamu ya pili ya uchaguzi wa wabunge inafanyika kama ilivyopangwa

Amesema Umoja wa Mataifa kwa upande wake utaendelea kusaidia mamlaka hizo za mpito ili kuhakikisha kipindi cha mpito kinakamilika tarehe 31 Machi kama ilivyopangwa.