Skip to main content

Ban asema ana imani na wana Comoro katika uchaguzi wa kesho

Ban asema ana imani na wana Comoro katika uchaguzi wa kesho

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha hatua iliyofikiwa visiwani Comoro katika maandalizi ya awamu ya kwanza ya uchaguzi wa Rais nchini humo, halikadhalika awamu ya kwanza ya uchaguzi wa magavana wa visiwa vya Comoro Kuu, Anjouan na Moheli.

Uchaguzi huo unafanyika kesho Jumapili tarehe 21 mwezi wa Februari ambapo awamu ya kwanza itawezesha kupatikana washindi watakaochuana kwenye awamu ya pili mwezi Aprili.

Ban katika taarifa ya msemaji wake ameripotiwa akisema kuwa wananchi wa Comoro wana wajibu wa pamoja wa kuhakikisha chaguzi hizo zinafanyika kwa amani, uwazi na zinakuwa halali.

Amesema Umoja wa Matafia kwa ushirikiano na wadau wengine wa kimataifa nchini Comoro wataendelea kusaidia wananchi hao katika jitihada zao za kujenga demokrasia, amani na kuendeleza maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Kwa mujibu wa katiba ya nchi, kiti cha urais nchini Comoro kinazunguka katika visiwa hivyo vitatu ambapo awamu hii ni zamu ya Comoro Kuu.