Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMAS yazindua mpango kazi dhidi ya mabomu ya kutegwa ardhini

UNMAS yazindua mpango kazi dhidi ya mabomu ya kutegwa ardhini

Idara ya Umoja wa Mataifa ya kuchukua hatua dhidi ya mabomu ya kutegwa ardhini UNMAS imezindua mpango kazi kwa mwaka 2016 wenye thamani ya dola milioni 357.

Mahitaji ya UNMAS ambayo yanalenga kutekeleza miradi kwenye sehemu 23 duniani yameongezeka yakilinganishwa na mwaka 2015 ambapo mahitaji yalikuwa ni dola milioni 286 tu.

Akihutubia kikao maalum kilichofanyika leo mjini Geneva Uswisi, mkuu wa UNMAS Agnes Marcaillou amesema kwamba usaidizi wa kibinadamu hauwezi kufanikiwa iwapo hautatanguliwa na hatua thabiti dhidi ya mabomu ya kutegwa ardhini.

Ameeleza kwamba dunia ya leo inakumbwa na vita ambavyo wapiganaji wake hawaheshimu sheria ya kimataifa wakilenga moja kwa moja raia, hospitali, mashirika yasiyo ya kiserikali na Umoja wa Mataifa.

Bi Marcaillou amesisitiza kwamba maisha ya watu yanayohatarishwa na mabomu ya kutegwa ardhini hayawezi kusubiri ufadhili ili kuokolewa.