Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM walaani mauaji na uharibifu katika kituo cha ulinzi wa raia Malakal

UM walaani mauaji na uharibifu katika kituo cha ulinzi wa raia Malakal

Mratibu wa kibinadamu nchini Sudan Kusini, Eugene Owusu, amelaani mauaji ya angalau watu 18, wakiwemo wahudumu wawili wa kibinadamu, pamoja na uharibifu wa vifaa vya kibinadamu na makazi ya raia kwenye kituo cha ulinzi wa raia mjini Malakal, Sudan Kusini.

Akieleza kutiwa huzuni na tukio hilo, Bwana Owusu ametuma risala za rambi rambi kwa familia za waliouawa na kutoa wito waliotekeleza ghasia hizo wakabiliwe kisheria, huku akiwasihi wenye ushawishi wahakikishe utulivu unarejeshwa.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kituo hicho cha ulinzi wa raia kilizinduliwa kama hifadhi salama kwa watu wanaokimbia ili kuokoa maisha yao, na kamwe haikubaliki kwamba kituo hicho sasa kimekuwa mahali wanakouawa watu na kujeruhiwa.

Kabla ya ghasia hizo, kituo hicho cha ulinzi wa raia cha Malakal kilikuwa kinawapa hifadhi wakimbizi wa ndani 47,000.