Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usalama wa wahamiaji na wakimbizi uimarishwe baharini:UM

Usalama wa wahamiaji na wakimbizi uimarishwe baharini:UM

Wastani wa watoto wawili hufa maji kila siku kuanzia Septemba mwaka jana wakati familia zao zikijaribu kuvuka bahari ya Mediterranean kuelekea Ulaya. Idadi ya vifo vya watoto inaongezeka kwa mujibu wa shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, shirika la kimataifa la uhamiaji IOM na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF. Joshua Mmali na ripoti kamili.

 (Taarifa ya Joshua)

 Mashirika hayo yametoa wito wa kuimarishwa usalama wa wale wote wanaokimbia machafuko na wako katika taharuki.

Yameongeza kuwa tangu Septemba mwaka jana wakati kifo cha mtoto Aylan Kurdi kilichoutia simanzi ulimwengu zaidi ya watoto 340, wengi wakiwa wadogo sana wamekufa maji kwenye bahari ya Mediterranean.

Akizungumzia hali hiyo mkurugenzi mkuu wa UNICEF Anthony Lake amesema hawawezi kufumbia macho zahma hii kwa mamia ya maisha ya watoto wasio na hatia na kupoteza taifa la baadaye au kushindwa kushughulikia hatari ambayo inawakabili maelfu ya watoto wengine.

Ameongeza inawezekana ikashindikana kumaliza chanzo cha mamilioni ya watu kukimbia na kuvuka bahari kwa sasa lakini nchi zinaweza na ni lazima zishirikiane kuhakikisha safari hiyo ya hatari inakuwa salama.