Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika inapata hasara kubwa kwa wizi wa kuhamishia fedha ng’ambo- Mbeki

Afrika inapata hasara kubwa kwa wizi wa kuhamishia fedha ng’ambo- Mbeki

Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, ambaye pia ni mwenyekiti wa jopo la ngazi ya juu kuhusu uhamishaji haramu wa fedha kutoka barani Afrika, amesema kuwa hatua madhubuti ni lazima zichukuliwe hima ili kukabiliana na tatizo la kuhamishia ng’ambo fedha kwa njia haramu.

Bwana Mbeki amesema hayo katika mahojiano na Redio ya Umoja ya Mataifa, baada ya kikao cha jopo hilo kuhusu uhamishaji haramu wa fedha kutoka Afrika, ambacho kimefanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York.

Bwana Mbeki amesema alipochukua wadhfa wa mwenyekiti wa jopo hilo, alishangaa alipogundua kuwa uhalifu huo wa kuhamishia ng’ambo fedha zinazoibwa kutoka serikalini ulikuwa unafanyika kwa kiwango kikubwa sana.

(Sauti ya Mbeki)

“Ni lazima tuchukue hatua, kwani bara letu linapata hasara sana kutokana na uhamishaji huu haramu wa fedha.Kama nchi za Afika, serikali zetu zinapaswa kujenga uwezo wa kufuatilia kinachofanyika katika gharama za biashara, ili kusiwe na watu wanaoagiza bidhaa kutoka ng’ambo halafu wanawasilisha ankara zinazoonyesha bei ya juu kuliko ilivyo kweli. Tunapaswa kuhakikisha kuwa mamlaka za forodha zina uwezo wa kutambua hilo.”