Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Misaada ya kibinadamu Syria kudondoshwa kutoka angani – ISSG

Misaada ya kibinadamu Syria kudondoshwa kutoka angani – ISSG

Kikosi kazi kinachoongozwa cha kimataifa kinachosaka kufikishwa kwa misaada ya kibinadamu nchini Syria, ISSG kimehitimisha mkutano wake huko Geneva, Uswisi leo na kusema misaada itaanza kudondoshwa kutoka angani ili kufikia wakazi wa eneo la Deir ez-Zour linaloshikiliwa na ISIL.

Kikao hicho kimeamua kupatia kipaumbele eneo hilo kwanza na baadaye kusaka kufikia mamilioni ya watu wengine walioko maeneo ambayo si rahisi pia kufikiwa kwenye nchi hiyo iliyoko vitani.

Jan Egeland ambaye ni mwenyekiti mwenza wa kikosi kazi hicho ambacho Umoja wa Mataifa pia ni mjumbe amethibitisha misaada imefikia watu 80,000 siku ya Jumatano lakini kuhusu eneo la Dair ez-Zour lenye wakazi 200,000...

(Sauti ya Egeland)

 “Njia pekee ni kudondosha misaada kutoka angani. WFP ina mipango thabiti ya kufanya hivyo. Wajumbe wengi wa kikao wameahidi kuunga mkono operesheni hiyo na imedhihirishwa kuwa katika fursa nyingi ya kikao kuwa wenyeviti wenza ambao ni Marekani na Urusi wamekuwa na ushirikiano mzuri.”

Bwana Egeland amesisitiza kuwa ni muhimu kuendelea kuhakikisha misafara yenye misaada ya kibinadamu inafikia walengwa kwani misaada iliyowasilishwa Jumatano inatosha kwa mwezi mmoja tu.