Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulaya dhihirisheni utetezi wenu wa haki za binadamu- Crépeau

Ulaya dhihirisheni utetezi wenu wa haki za binadamu- Crépeau

Wakati viongozi wa muungano wa ulaya wakikutana kuanzia leo huko Brussels, Ubelgiji mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za wahamiaji François Crépeau, amewataka waonyeshe wajibu wa kisiasa na kimaadili kupiga vita chuki dhidi ya wageni.

Amesema hayo akizingatia kuwa kila uchao yaonekana imekuwa vigumu kwa chombo hicho kuwa na mjadala wa maana na kuafikiana kuhusu haki za wahamiaji, utangamano na ujumuishi.

Katika taarifa iliyotolewa na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, Bwana Crépeau amesema mwelekeo wa sasa dhidi ya wageni unatia shaka wakati Ulaya imekuwa mtetezi wa haki za binadamu barani humo na hata kwingineko duniani.

Amesema wakati huu ambapo Ulaya inahaha kudhibiti mipaka yake,ni jaribio kubwa kwa ukanda huo katika uzingatiaji wa haki za binadamu na kudhihirisha utetezi wake wa haki kwingineko.

Bwana Crépeau amesema kwa kitendo cha Ulaya kupokonya taratibu haki za wahamiaji na wasaka hifadhi kwa kujengea hofu wananchi wao, kinaweka hali ya shaka ambayo inaonekana taratibu ya kawaida.