Skip to main content

El Niño kali imepita lakini madhara yake kuendelea – WMO

El Niño kali imepita lakini madhara yake kuendelea – WMO

Shirika la hali ya hewa duniani, WMO limesema msimu mkali wa El Nino kwa mwaka 2015-2016 umepita lakini bado itasalia kuathiri mabadiliko ya tabianchi ulimwenguni.

WMO imesema El Nino inatarajiwa kudhoofika miezi michache ijayo na hatimaye kutokomea robo ya pili ya mwaka huu, lakini ni vyema kuwa macho kwani madhara yake kibinadamu na kiuchumi yanaendelea kudhihirika.

Katibu Mkuu wa WMO Petteri Taalas amesema dunia imeshuhudia hali ya hewa mbaya zaidi kuwahi kusababishwa na El Nino iliyochochoea kiwango cha joto mwaka 2015 kuvunja rekodi na kuleta ukame na mafuriko maeneo mbali mbali.

Amesema maeneo kama ya pembe ya Afrika bado yanajikwamua kutokana na madhara ya El Nino ikizingatiwa ukame uliokumba eneo hilo.

Amesema kile ambacho wamejifunza kutokana na mwelekeo huo wa hali ya hewa kitatumika kujenga mbinu bora zaidi za kuhimili majanga yatokana na hali ya hewa ambayo yataongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi.