Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka 2016 ni lazima tusonge mbele kwa vitendo kuhusu tabianchi- Ban

Mwaka 2016 ni lazima tusonge mbele kwa vitendo kuhusu tabianchi- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema mkataba kuhusu mabadiliko ya tabianchi uliopitishwa jijini Paris Disemba mwaka jana, unatoa msingi imara wa kuendeleza uchumi wa kimataifa kwa njia inayozalisha hewa ndogo ya mkaa na inayohimili tabianchi.

Akihutubia nchi wanachama wa Umoja huo kuhusu hafla ya kutia saini mkataba huo ambayo itafanyika Aprili 22 mwaka huu, Ban amesema mkataba huo utawezesha kuongeza msukumo mara kwa mara, ambao unahitajika ili kuhakikisha ongezeko la joto duniani linasalia chini ya nyuzi joto mbili kwenye kipimo cha selsiasi, akisema mkataba huo ...

"Utawezesha kutunza mustakhbali salama, ulio bora na wenye ufanisi zaidi kwa watu wote. Lakini kazi bado. Ama hakika, ndio sasa imeanza. Mwaka huu wa 2016, ni lazima tusonge mbele na kugeuza maneno kuwa vitendo.”

Katibu Mkuu ameongeza kwamba hafla ya utiaji saini Mkataba wa Paris itakuwa hatua muhimu.

“Itakuwa siku ya kihistoria. Hafla ya kutia saini mkataba itakuwa fursa ya kwanza kwa serikali kuendeleza mchakato utakaopelekea utekelezaji na kuridhia Mkataba wa Paris. Ushiriki wa viongozi wa nchi na serikali utaonyesha dunia kuwa wana dhamira ya kusonga mbele haraka iwezekanavyo.”

Ban amesisitiza umuhimu wa kuanza kuutekeleza Mkataba wa Paris haraka, akiongeza kwamba madhara ya kutochukua hatua yanakuwa dhahiri kila uchao. Ametoa mifano ya majanga ya hali ya hewa, mathalani mvua nzito na mafuriko, ukame, kupanda viwango vya maji baharini, watu kufariki dunia, kupoteza nyumba na vitega uchumi na hatimaye kupoteza matumaini.