Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila mlinda amani anapaswa kuwa mlinzi wa walio hatarini- Eliasson

Kila mlinda amani anapaswa kuwa mlinzi wa walio hatarini- Eliasson

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson, amesisitiza haja ya kuhakikisha kuwa walinda amani wanatimiza viwango vya juu zaidi vya tabia na nidhamu wakati wanapoendesha operesheni zao.

Bwana Eliasson amekuwa akihutubia kamati maalum ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu operesheni za ulinzi wa amani, ambayo iliundwa mnamo mwaka 1965 kufanyia tathmini ya kina masuala yote yanayohusu ulinzi wa amani.

Hili ni muhimu iwapo tunataka kutunza uaminifu wa jitihada zetu za ulinzi wa amani. Sote tumeshuhudia jinsi vitendo viovu vinavyoweza kuuletea ulinzi wa amani jina baya. Kila mlinda amani anapaswa kuwa mlinzi. Kuwanyanyasa walio hatarini ni usaliti kwa imani hiyo. Panapoibuka visa vya unyanyasaji wa kingono, ni lazima kuwepo uwajibikaji haraka. Hili ni jukumu la Umoja wa Mataifa, na pia la nchi wanachama.”

Bwana Eliasson amesema, mizozo imechukua sura mpya nyakati za sasa, na hivyo kuweka shinikizo kubwa kwa jamii ya kimataifa na wadau wote.

Walinzi wa amani wanafanya kazi katika mazingira hatarishi hata zaidi. Makundi yenye itikadi kali na katili hunawiri penye vurugu na machafuko. Mashambulizi ya kulenga hufanywa dhidi ya walinda amani wetu, kama vile lile la Ijumaa iliyopita kaskazini mwa Mali. Mifumo yetu iliyopo aghalabu haimudu changamoto hizi mpya. Lakini uwezo uliothibitishwa wa ulinzi wa amani katika Umoja wa Mataifa kubadilika na kuendana na mahitaji mapya ni moja ya nguvu zetu kubwa zaidi.”

Hata hivyo, Bwana Eliasson amesema kuwa shughuli za ulinzi wa amani katika Umoja wa Mataifa siyo chombo cha kuendeleza masuluhu ya kijeshi kwa mizozo, bali ni chombo cha kuendeleza masuluhu ya kisiasa.