Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasifu wa Boutros Boutros-Ghali - Daima atakumbukwa kwa mchango wake UM

Wasifu wa Boutros Boutros-Ghali - Daima atakumbukwa kwa mchango wake UM

Boutros Boutros-Ghali, Katibu Mkuu wa sita wa Umoja wa Mataifa ameaga dunia hii leo akiwa na umri wa miaka 93. Alizaliwa Novemba 14 mwaka 1922 mjini Cairo Misri akitoka katika familia tajiri yenye ushawishi mkubwa na ya Wakristo wa dhehebu la Coptic.

Akizungumzia kifo chake Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon amesema amestushwa sana . Bwana Ghali alikuwa mtu aliyeheshimiwa na taifa lake la Misri, mwanazoni  lakini pia kiongozi shupavu aliyeupitisha Umoja wa mataifa katika kipindi cha changamoto nyingi.

(SAUTI YA BAN)

“Boutrous Boutrous –Ghali alifanya mengi kwa taswira ya umoja huu katika wakati huu, hususani katika ripoti yake ya kihistoria nanukuu”ajenda kwa ajili ya Amani”uwajibikaji wake kwa umoja wa Mataifa, mipango yake na mambo yake sio vya kukosea, na kovu aliloliacha kwenye Umoja huu halifutiki.Jumuiya ya Umoja wa mataifa itamuumboleza kiongozi aliyetoa huduma muhimu kwa ajili ya utulivu na amani ya dunia.”
Uongozi ulikuwa damuni kwa Bwana Ghali, kwani Baba yake Yusuf Ghali aliwahi kuwa waziri wa fedha wa Misri na ingali babu yake alikuwa waziri mkuu wa taifa hilo kuanzia mwaka 1908 hadi alipouawa mwaka 1910.

Boutrous-Ghali aliyekuwa mtanashati na mzungumzaji wa lugha mbalimbali ikiwemo Kiingereza, kifaransa na Kiarabu alisomea sheria kwenye chuo kikuu cha Cairo na baada ya kuhitimu mwaka 1946 akahamia Ufaransa kwa miaka minne akijikita katika kusoma masuala ya kidiplomasia na uchumi na hatimaye kupata shahada ya uzamivu au Phd ya sheria za kimataifa kwenye chuo kikuu cha Paris mwaka 1949.

Alikuwa miongoni mwa wajumbe wa tume ya Umoja wa mataifa ya sheria za kimataifa kuanzia mwaka 1979-1992, na ndipo alipopata fursa ya kuyafahamu vizuri masuala ya Umoja wa Mataifa ambayo baadaye yalimpa fursa ya kutumikia Umoja huo hapo baadaye.

Lakini kwanza alitumikia taifa lake kama waziri wa mambo ya nje enzi za utawala wa Rais Anwar Sadat. Na alipoingia madarakani Rais Hosni Mubarak alimpandisha cheo na kumfanya kuwa naibu waziri mkuu wa masuala ya kimataifa hadi pale alipopata mwaliko rasmi wa kuungoza Umoja wa Mataifa mwinshoni mwa mwaka 1991.

Bwana Boutros-Ghali aliitikia wito na tarehe 3 Disemba mwaka 1991 aliapishwa Rasmi na Rais wa baraza kuu wakati huo Samir S. Shihabi wa Saudi Arabia ili  kushika wadhifa wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

(SAUTI YA BOUTROUS GHALI)

Mimi Boutros Boutrous- Ghali naapa kwamba nitatekeleza kwa heshima, uaminifu busara na ufahamu kazi niliyokabidhiwa mimi kama katibu mkuu wa Umoja wa mataifa."

Na majukumu yake yakaanza mnamo Januari mosi mwaka 1992 hadi Disemba 31 mwaka 1996. Alikuwa ni Mwarabu wa kwanza kuwahi kushika wadhifa huo, lakini pia ni Katibu Mkuu pekee kushika wadhifa huo kwa miaka mitano pekee.

Katika utawala wake Umoja wa Mataifa ulifanya mkutano wa kwanza wa baraza la usalama baada ya vita baridi tarehe 31 Januari 1992. Na ajenda kwa ajili ya amani ikazaliwa.

Huo ulikuwa ni mwanzo tu wa mengi aliyoyafanya ikiwemo kuanzishwa kwa kikosi maalumu cha ulinzi kwa ajili ya Yugoslavia ya zamani hapo Februiari 1992 (UNPROFOR) . Mwaka huohuo kukanzishwa operesheni maalumu ya kulinda amani Somalia baada ya kuangushwa kwa utawala wa Siad Barre (UNOSOM)

image
Hayati Boutros Boutros-Ghali ziarani nchini Somalia. (Picha:UN/Milton Grant)

Viongozi wa dunia aliwakutanisha Brazili kwa ajili ya mkutano wa Umoja wa mataifa wa mazingira na maendeleo. Sheria yake ikaanza kushika mkondo pale alipoanzisha mahakama ya kwanza kabisa ya Umoja wa mataifa ya uhalifu wa kivita ICTY mnamo Mai 25 mwaka 1993, lengio likiwa kuhukumu walioshukiwa kuuwa maelfu ya watu huko Balkans.

Tarehe 24 Septemba mwaka 1993 chini ya uongozi wake mpango maalumu wa msaada wa Umoja wa Mataifa ulianzishwa nchini Rwanda (UNAMIR) kwa lengo la kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya serikali ya mpito, lakini mambo yakachahca mwaka 1994 na mauaji ya kimbari yakazuka kwa siku 100, watu Zaidi ya 800,000 wakapoteza maisha.

Na Bwana Ghali alishuhudia pia juhudi za miongo mine ya Umoja wa Mataifa zikizaa matunda Afrika ya Kusini hapo April 26 mwaka 1994 ulipofanyika uchaguzi mkuu wa kwanza uliojumuisha rangi zote na Nelson Mandela aliyeachiwa kifungoni baada ya miaka 27 akaibuka kidedea.

image
Hayati Boutros Boutros-Ghali akiwa na mwenda zake Nelson Mandela, rais wa Afrika Kusini. (Picha:UN/Milton Grant)

Ghali alihakikisha waliotekeleza mauaji ya kimbari ya Rwanda wafikishwa kwenye mkono wa sheria alipoidhinisha kuanzishwa kwa mahakama ya kimataifa ya mauji ya kibari ya Rwanda ICTR hapo Februari 22 mwaka 1995, ilioingia katika historia kama mahakama ya kwanza kuhukumu waliohusika na mauaji hayo lakini pia kama taasisi ya kwanza kutambua ubakaji kama njia ilinachochea mauaji ya kimbari

image
Panga na risasi mpakani mwa Gisenyi nchini Rwanda mwaka 1994(Picha:UM/J. Isaac)

Na kabla ya kuondoka madarakani Disemba 31 mwaka 1996 bwana Ghali alizuru Kuwait mpango wa Amani wa Umoja wa Mataifa ambao ulijitahidi kukomesha uvamizi wa Iraq katika ttaifa hilo. Lakini makubwa mengine atakayokumbukwa nayo daima ni kuanzisha ajenda ya maendelo kwa ajili ya kuboresha maisha ya binadamu, kuuita ukatili dhidi ya wanawake kuwa ni tatizo la kimataifa linalohitaji kulaaniwa kimataifa na kushuhudia mkutano wa kwanza wa kimataifa wa wanawake huko Beijing 1995 na akafunga pazia kwa azimio maalumu la kupinga majaribio ya nyuklia ambalo hadi leo linaendelea kuliridhiwa.

Wanadiplomasia waliomfahamu Bwana Ghali watamkumbuka kwa mengi , miongoni mwao ni Ahmed Fawzi aliyewahi kuwa naibu Katibu Mkuu wake na sasa ni msemaji wa ofisi ya umoja wa Mataifa Geneva

(SAUTI YA FAWZI)

Boutrous Boutrous –Ghali alikuwa mtu mwenye kujiami sana kwa kuwa , mmisri, mkristo, kwa  kutumia taifa lake na jumuiya ya kimataifa alipokuwa Katibu Mkuu. Nadhani jukumu kubwa kwa jumuiya ya kimataifa …………….ni pale aliposimamia uhuru wa ofisi yake ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, na huo ni utamaduni natumai tutaushuhudia ikienziwa siku za usoni.

Boutros Boutros-Ghali ameacha mume na watoto, daima atakumbukwa.