Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia wa Syria wanakumbana na hali ngumu ya afya- WHO

Raia wa Syria wanakumbana na hali ngumu ya afya- WHO

Shirika la Afya Duniani, WHO, limesema kuwa hali nchini Syria inaendelea kuzorota, hususan katika miji ya Aleppo, Azaz na kaskazini mwa Homs vijijini.

Kwa mujibu wa WHO, vituo vinne vya afya vilikuwa vimeharibiwa katika mashambulizi ya angani kufikia jana. WHO imesema mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya vituo vya afya yana madhara makubwa ya moja kwa moja na ya muda mrefu, kwani yanawanyima watu walio hatarini huduma muhimu za kuokoa maisha, hususan watoto.

Aidha, WHO imesema zaidi ya wahudumu 640 wa afya wameuawa tangu mzozo wa Syria ulipoanza, na kwamba takriban asilimia 58 ya hospitali zote za umma na asilimia 49 ya vituo vya afya ama vimefungwa, au vinatoa huduma kidogo sana.

Wengi wa raia wa Syria, wakiwemo waliosaka hifadhi katika nchi jirani, wamo katika hatari ya kukumbwa na magonjwa.