Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Boutros Boutros-Ghali afariki dunia

Boutros Boutros-Ghali afariki dunia

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limekutana leo kuhusu hali Mashariki ya Kati na Yemen, ambapo pia rais wa Baraza hilo ametangaza kifo cha aliyekuwa Katibu Mkuu, Boutros Boutros-Ghali. Taarifa kamili na  Joshua Mmali

(Taarifa ya Joshua)

Ni Rais wa Baraza la Usalama Balozi Rafael Darío Ramírez Carreño wa Venezeua, akitangaza kifo cha aliyekuwa Katibu Mkuu Boutros Boutros-Ghali,  ambaye amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 93. Boutros-Ghali alihudumu kama Katibu Mkuu kati ya mwaka 1992 na 1996.

Baraza hilo limekutana kumulika hali Mashariki ya Kati na kufanya mashauriano kuhusu Yemen, kikihutubiwa na Mratibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu katika Umoja wa Mataifa, Stephen O’Brien.

Bwana O’Brien amesema mzozo wa Yemen unaendelea kuwaua na kuwalemaza raia, ukisababisha maafa makubwa na kuharibu uchumi, majumba, misingi ya jamii na miundo mbinu muhimu

“Uharibifu mwingi unatokana na mashambulizi holela ya mabomu na makombora kutoka pande kinzani. Tangu Machi 2015, zaidi ya wahanga 35,000, vikiwemo zaidi ya vifo 6,000, vimeripotiwa na vituo vya afya kote nchini. Mzozo unasababisha madhara makubwa ya kibinadamu.Watu wapatao milioni 2.7 wamekimbia makwao”