Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mbinu za zamani na za kisasa za kudhibiti mbu wa Zika ziimarishwe- WHO

Mbinu za zamani na za kisasa za kudhibiti mbu wa Zika ziimarishwe- WHO

Wakati baraza la uchumi na kijamii la Umoja wa Mataifa likikutana baadaye leo kujadili virusi vya Zika, shirika la afya ulimwenguni, WHO limetoa andiko lake linalopendekeza matumizi ya pamoja ya mbinu mpya na za zamani za kutokomeza  mbu aina ya Aedes Aegypti anayeeneza virusi hivyo. Flora Nducha na ripoti kamili.

(Taarifa ya Flora)

Pendekezo hilo la WHO linazingatia hofu ya sasa ya kuzidi kuenea kwa virusi hivyo ambavyo vinahusishwa na watoto kuzaliwa na vichwa vidogo na hata mambukizi kwa njia ya ngono.  Hofu pia inazingatia kuwa itachukua miezi hadi 18 kuweza kupata chanjo ya majaribio kwa watu wengi dhidi ya Zika.

Katika andiko lake WHO linasema mbinu za zamani kama vile kupulizia dawa, kuondoa madimbwi ya maji na hata kupaka dawa za kufukuza mbu ziende sambamba na mbinu mpya.

Mbinu hizo ni pamoja na mbu dume kupigwa miali ambapo anapokutana na mbu jike mayai yanayotagwa hayana uwezo kutoa vimelea na hivyo mbu hao wanatoweka na ile ya kuwa na mbu ambaye jeni zake zimeboreshwa na hii bado inafanyiwa tathmini.

WHO imetaka serikali kutobweteka na kupatia ufadhili wa kutosha mbinu za kujikinga dhidi ya mbu kwani kulikopatikana mafanikio, mipango hiyo imekufa au imedorora.