Skip to main content

Tuna hofu na msako wa China dhidi ya wanaharakati- Zeid

Tuna hofu na msako wa China dhidi ya wanaharakati- Zeid

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein amesema anazidi kutiwa hofu na jinsi China inavyofanya msako dhidi ya wanasheria na wanaharakati nchini humo wakiwemo wanaokosa serikali. John Kibego na taarifa kamili.

(Taarifa ya Kibego)

Zeid amesema kitendo cha serikali kinatia shaka hasa kwa kazi njema inayofanywa na makundi hayo ilhali ni wajibu wa serikali kuwalinda.

Amesema mazungumzo yake na maafisa wa China kuhusu shaka hiyo walipokutana Geneva, Uswisi yamedokeza kuwa mara nyingi serikali inakamata watetezi wakikanganya wajibu wa kisheria wa makundi hayo na madai kuwa wanatishia ulinzi na usalama wa raia.

Rupert Colville ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu Geneva.

(Sauti ya Rupert)

"Wanasheria hawapaswi kuwa wahanga wa mashtaka, vikwazo au kutishiwa kwa ajili ya kuendeleza kazi zao, badala yake wana  jukumu muhimu la kulinda haki za binadamu na sheria na kamishna mkuu ametoa wito kwa serikali ya Uchina waachiwe huru mara moja bila masharti."

Mwezi uliopita wanasheria 15 walikamatwa, 10 kati yao kwa tuhuma za uhaini kosa ambalo adhabu yake ni kati ya kifungo cha miaka 15 jela hadi kifungo cha maisha.