Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ajenda za Baraza la Usalama zisibebwe kijiografia au kiushandani- Ban

Ajenda za Baraza la Usalama zisibebwe kijiografia au kiushandani- Ban

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao kuhusu kuendeleza amani na  usalama duniani ikiangazia umuhimu wa  kuheshimu misingi na malengo ya katiba iliyoanzisha Umoja huo miaka 70 iliyopita. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Nyaraka ya kuitishwa kikao hicho iliyotolewa na Venezuela ambayo ndiyo Rais wa baraza hilo kwa mwezi huu wa Februari imezingatia misingi ya katiba ambayo ni usawa baina ya mataifa, na kila nchi kuheshimu mamlaka na utaifa wa nchi kama njia ya kuendeleza ushirikiano wa kimataifa.

Akihutubia Ban amesema kikao cha leo kinaendeleza mjadala ulioanzishwa mwaka jana kuhusu kusimamia misingi ya katiba ya Umoja wa Mataifa hata wakati wa kuamua hatua za kuchukua kudhibiti migogoro na kuendeleza amani.

Amegusia ibara ya 99 ya Katiba ya Umoja huo kuhusu Katibu Mkuu kuwasilisha hoja mbele ya Baraza la usalama iwapo kuna suala linalotishia usalama duniani akisema..

(Sauti ya Ban)

“Wakati tunaangalia ni suala gani linakidhi ajenda ya Baraza la Usalama, ni matumaini yangu kuwa tutakuwa tunachochewa na misingi ya Katiba ya Umoja wa Mataifa na siyo ushindani kutoka maeneo yetu ya kijiografia au mashinikizo yoyote ya nje.”

Ban amesema Baraza la Usalama lina nyenzo nyingi za kuendeleza amani na usalama duniani lakini jambo la msingi ni umoja ndani ya chombo hicho ili hatimaye kiweze kutatua mizozo kabla haijaota mizizi.