Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uingereza na Sweden tekelezeni uamuzi kuhusu Assange - Wataalamu

Uingereza na Sweden tekelezeni uamuzi kuhusu Assange - Wataalamu

Mtaalam huru wa Umoja wa Mataifa Alfred de Zayas amezitaka Uingereza na Sweden kutekeleza bila kuchelewa uamuzi na mapendekezo ya jopo la Umoja huo kuhusu kushikiliwa kwa mwanzilishi wa mtandao wa WikiLeaks Julian Assange.

Jopo hilo kuhusu ushikiliwaji wa watu kiholela lilibaini kuwa Assange anashikiliwa kiholela na hivyo likatoa wito kwa Sweden na Uingereza kumaliza hali ya kunyimwa uhuru na pia kumwezesha haki yake ya kulipwa fidia.

De Zayas ametaka uamuzi huo kutekelezwa kwa nia njema akisema kuwa hali ya uendelevu na amani duniani inataka nchi kuheshimu, kuendeleza na kuzingatia haki za binadamu sanjari na kuwajibika kwa mapendekezo ya vyombo vya haki.

Amesema iwapo nchi inazingatia haki za binadamu, haiwezi kuweka ukomo wa haki hizo kwa kuchagua kile inachotaka kufanya na kwamba watoa taarifa ni watetezi muhimu wa haki za binadamu katika karne hii ya 21 ambayo usiri na ukosefu wa taarifa unasababisha ukiukwaji wa haki.