Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban atoa wito awamu ya pili ya uchaguzi CAR ifanyike kwa amani

Ban atoa wito awamu ya pili ya uchaguzi CAR ifanyike kwa amani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ametoa wito kwa raia wote wa Afrika ya Kati, wakiwemo wagombea wa urais na ubunge, kuhakikisha kuwa awamu ya pili ya uchaguzi wa rais na uchaguzi mpya wa wabunge uliopangwa kufanyika hapo kesho Februari 14 unafanyika kwa njia ya amani na inayoaminika.

Katibu Mkuu amezipongeza mamlaka za mpito kwa juhudi zinazolenga kumaliza kipindi cha mpito wa kisiasa ifikapo Machi 31, 2016, akisema kuwa uchaguzi huo wa Jumapili utaisongesha nchi hiyo karibu na ukomo wa mpito na kurudia utawala wa kikatiba.

Ameutaja uchaguzi huo kama hatua muhimu kuelekea ustawi wa kisiasa na kujikwamua kiuchumi kwa mtazamo mrefu.

Aidha, Katibu Mkuu amekumbusha mchango muhimu unaotolewa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa CAR, MINUSCA, kwa mchakato huo wa uchaguzi, akikariri dhamira ya ujumbe huo kuchukua hatua zote zifaazo ili kuzuia kuvurugika kwa uchaguzi huo.