Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utumikishwaji watoto vitani bado ni tatizo DRC

Utumikishwaji watoto vitani bado ni tatizo DRC

Leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya watoto wanaotumikishwa vitani, ikijulikana pia kwa jina la siku ya mkono mwekundu, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, MONUSCO umeandaa mafunzo ya uhamasishaji mjini Beni, Kivu Kaskazini.

Zaidi ya watoto 600 wameshiriki mafunzo hayo, pamoja na viongozi wa serikali na jeshi na wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na MONUSCO.

MONUSCO imeeleza kwamba, kutokana na hali ya usalama Kivu Kaskazini, ilikuwa ni lazima kuwafundishia watoto kuhusu utumikishwaji wa watoto vitani na ukatili wa kingono, Meya wa Beni akiongeza kwamba vikundi kadhaa vya waasi vinaendelea kuajiri watoto na kuwafundishia jinsi ya kuua binadamu.

Kwa mujibu wa takwimu za ofisi ya ulinzi wa watoto Beni, mwaka 2015, watoto 17 waliokolewa kwenye eneo la Beni baada ya kutumikishwa vitani na waasi, , huku wengine 23 wakiwa wameuawa.