Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwelekeo Mashariki ya Kati wahatarisha suluhu ya mataifa mawili

Mwelekeo Mashariki ya Kati wahatarisha suluhu ya mataifa mawili

Wawakilishi wa kundi la pande nne ambazo ni Muungano wa Ulaya, Urusi, Marekani na Umoja wa Mataifa, lijulikanalo kwa kiingereza kama Quartet wamekutana leo Ujerumani kuzungumzia hali ya usalama Masharili ya kati.

Wawakilishi hawa akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson wamelaani vitendo vyote vya ugaidi na kuelezea wasiwasi wao kuhusu ghasia inayoendelea dhidi ya raia kwenye eneo hilo, wakitoa wito kwa pande kinzani kuchukua hatua kupunguza mvutano.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema Quartet inahofia kwamba mwelekeo wa ghasia, ikiwa ni mashambulizi dhidi ya raia, uteketezaji wa nyumba za wapalestina na ujenzi wa walowezi wa Israel ambao ni kinyume na sheria, huenda ukahatarisha uwezekano wa kutekeleza suluhu ya mataifa mawili.

Wawakilishi hao wamesisitiza utashi wao wa kushirikiana ili kurejesha utulivu, na kutafuta suluhu ya kudumu kwa mzozo kati ya Palestina na Israel.