Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yataka wagombea Urais CAR kujali maslahi ya watoto

UNICEF yataka wagombea Urais CAR kujali maslahi ya watoto

Wakati ambapo awamu ya pili ya uchaguzi wa rais na wabunge inatarajiwa kufanyika jumapili hii nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF limetoa wito kwa wagombea kuweka kipaumbele suala la watoto. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Geneva Uswisi, msemaji wa UNICEF Christophe Boulierac amesema watoto ndio waathirika wa kwanza wa mzozo unaoikumba nchi hii, akikariri wito wa shirika hilo..

(Sauti ya Bwana Boulierac)

“ Kitu muhimu zaidi kwetu ni kwamba rais mtarajiwa ahakikishe msaada kwa watoto uko juu kwenye ajenda. Katika hali hii ngumu, ni muhimu sana kumkumbusha rais mtarajiwa kwamba kutokana na takwimu za kushtua, kusaidia watoto ni kuendeleza mustakabali wa nchi na hakuwezi kuwa chaguo la pili. "

Bwana Boulierac amesema asilimia 45 ya watoto chini CAR wanakumbwa na utapiamlo na theluthi moja hawaendi shuleni, huku karibu 10,000 wakiwa wametumikishwa vitani.