Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban alaani mashambulizi ya bomu dhidi ya wakimbizi wa ndani Nigeria

Ban alaani mashambulizi ya bomu dhidi ya wakimbizi wa ndani Nigeria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amelaani mashambulizi mawili ya bomu yaliyofanywa na watu wanaoshukiwa kuwa wafuasi wa Boko Haram mnamo Februari 9, dhidi ya kambi ya wakimbizi wa ndani ya Dikwa, jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Taarifa ya Msemaji wake imesema kuwa Ban amehuzunishwa na vifo vya makumi ya wakimbizi wa ndani katika mashambulizi hayo mawili, na kujeruhiwa kwa wengine wengi. Katibu Mkuu ametuma rambirambi zake kwa serikali, watu wa Nigeria na familia za wahanga, na kuwatakia majeruhi nafuu haraka.

Katibu Mkuu ametoa wito ukatili wote wa kigaidi na kidini ukomeshwe nchini humo, na kukariri ahadi ya uungaji mkono wa Umoja wa Mataifa kwa serikali ya Nigeria katika jitihada zake za kupambana na ugaidi.

Ametaka njia za kina zitumiwe kuzuia na kupambana na janga la ugaidi, na kukabiliana na vyanzo vyake, kulingana na sheria ya kimataifa ya kibinadamu, haki za binadamu, na wakimbizi.