Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubia wa asasi za kiraia umeleta kheri kwa wanaotumia madawa ya kulevya- UNODC

Ubia wa asasi za kiraia umeleta kheri kwa wanaotumia madawa ya kulevya- UNODC

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Madawa ya Kulevya na Uhalifu (UNODC), Yury Fedotov, amesema kuwa ubia kati ya shirika hilo na asasi za kiraia umekuwa ukiendeleza utoaji wa matibabu na huduma kwa watu wenye tatizo la uraibu wa madawa ya kulevya duniani.

Zaidi ya asasi 350 za kiraia zimepata usaidizi wa UNODC kuhusu kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi, matibabu, na usaidizi kwa watu wanaotumia madawa ya kudunga kwa sindano.

Bwana Fedotov amesema ushirikiano na asasi za kiraia umeongeza upatikanaji wa matibabu yanayozingatia haki katika zaidi ya nchi 40 kote duniani.

Mkuu huyo wa UNODC amesema hayo wakati wa hafla ya asasi za kiraia kuhusu mkutano maalum wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu tatizo la madawa ya kulevya duniani (UNGASS 2016), ambao utafanyika kuanzia tarehe 19 hadi 22 Aprili jijini New York.