Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jopo la wataalamu wa vikwazo Sudan laongezewa muda

Jopo la wataalamu wa vikwazo Sudan laongezewa muda

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo kwa kauli moja limepitisha azimio namba 2265 la mwaka 2016 la kuongeza hadi mwezi Machi mwakani muda wa jopo la wataalamu kuhusu vikwazo dhidi ya Sudan.

Azimio hilo limesema muda huo umeongezwa ili jopo hilo liweze kufanya kazi yake ya kufuatialia vikwazo dhidi ya Sudan kwa kuzingatia kuwa hali ya usalama nchini Sudan inaendelea kuwa tisho la usalama na usalama kwenye ukanda huo na duanini.

Azimio hilo limetaja vitisho na chuki dhidi ya raia huko Darfur na hivyo limetaja serikali ya Sudan kuendelea kupatia ushirikiano jopo hilo huku likieleza wasiwasi kuhusu shida inayopata jopo hilo katika kutekeleza mamlaka yake ikiwemo kufika

maeneo ambako kunaripotiwa ukiukwaji wa haki za binadamu.

Halikadhalika azimio linataka serikali ya Sudan kutekeleza ahadi zake ikiwemo kuondoa hali ya dharura huko Darfur na kuruhusu uhuru wa kujieleza sambamba na kuwajibisha wakiukaji wa haki za binadamu.

Jopo hilo la wataalamu limetakiwa kuripoti kwa Baraza la Usalama kila baada ya miezi mitatu kuhusu utendaji wake mathalani iwapo kuna vikwazo katika kufanya kazi yake na iwapo vikwazo dhidi ya Sudan vinakiukwa.