Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko ICAO kwa kanuni mpya kuhusu viwango vya uchafuzi angani

Heko ICAO kwa kanuni mpya kuhusu viwango vya uchafuzi angani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha tangazo la leo la shirika la masuala ya anga duniani, ICAO la kupendekeza viwango vya uchafuzi vinavyotolewa na vyombo vya usafiri angani ikiwemo ndege.

Taarifa ya msemaji wake imemnukuu Ban akisema kuwa kanuni hizo pendekezwa zitakazoweka ukomo wa hewa ya ukaa inayotolewa na ndege za kibiashara kuanzia mwaka 2028, zinaimarisha mipango ya kudhibiti mabadiliko ya tabianchi ikiwemo iliyoanzishwa  na mkataba wa mabadiliko ya tabianchi uliotiwa saini huko Paris, Ufaransa mwaka jana.

Ban amesema viwango vya hewa chafuzi kutoka sekta ya anga vinaongeza kwa kasi kubwa wakati huu ambapo idadi ya ndege za kibiashara inatarajiwa kuongezeka maradufu ifikapo mwaka 2030.

Kanuni hizo za ICAO zimekuja baada ya miaka kadhaa ya mashauriano na ni mara ya kwanza kwa serikali kuweka viwango kwa sekta hiyo ya anga.

Ban amesifu mpango huo huku akitoa wito kwa hatua zaidi kuimarisha viwango vya utoaji wa hewa chafuzi na hatua za kisayansi zichukuliwe.