Skip to main content

Kuchukua hatua katika usaidizi wa kibinadamu ni wajibu wa binadamu wote- Ban

Kuchukua hatua katika usaidizi wa kibinadamu ni wajibu wa binadamu wote- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amezindua ripoti yake kuhusu kongamano la kimatiafa la masuala ya kibinadamu litakalofanyika mwezi Mei mwaka huu huko Uturuki akisema binadamu wote wanawajibika kupunguza mateso ya mamilioni ya watu na kukabiliana na changamoto zinazoikumba dunia.

Akihutubia kikao kilichofanyika leo mjini New York Marekani kujadili ripoti hiyo Bwana Ban amesema changamoto za dunia ya leo zinazidisha uwezo wa nchi moja au taasisi moja wa kukabiliana nazo, akitoa wito kwa viongozi kuchukua hatua, na kusema

(Sauti ya Bwana Ban)

“Ni wajibu wa kimaadili na lazima ya kimkakati, Tusipozuia na kutatua mizozo, kuongeza uwezo wa kuhimili changamoto na kupunguza mateso hatutaweza kutimiza malengo yetu ya maendeleo endelevu. Watu kwenye mizozo wanataka tunachotaka sote: usalama, utu na fursa za kuchanua.”

Aidha Katibu Mkuu ameeleza mambo matano ya kupatiwa kipaumbele, ambayo ni kuzuia na kutatua mizozo, kuheshimu sheria ya kimataifa ya kibinadamu na haki za binadamu, kuhakikisha hakuna mmoja anayeachwa nyuma, kubadilisha mfumo wa usaidizi kwa kuimarisha uwezo wa watu wa kujitegemea, na kubuni mifumo mbadala ya ufadhili.