Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yawapatia vyakula wasyria wanaokimbia machafuko Aleppo

WFP yawapatia vyakula wasyria wanaokimbia machafuko Aleppo

Nchini Syria, Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP limeanza kusambaza vyakula kwa watu waliolazimika kuhama makwao kaskazini mwa Aleppo kufuatia kuongezeka kwa mapigano kwenye eneo hilo.

Msemaji wa WFP Bettina Luescher amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi kwamba usaidizi wa WFP umesafirishwa kupitia mpaka wa Uturuki na unalenga kufikia wakimbizi wa ndani 21,000.

Misaada hiyo ni vifurushi vya vyakula kama vile mchele, unga w a ngano, maharage, mafuta na sukari ambavyo vinaweza kutosha familia moja kwa mwezi mzima.

WFP imeeleza kwamba watu 30,000 zaidi wameripotiwa kukimbia mapigano Aleppo na kusaka hifadhi mpakani mwa Syria na Uturuki, huku machafuko yakihatarisha misafara ya mashirika ya kibinadamu kwenye eneo hilo.