Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

El-Niño na ukame yahatarisha upatikanaji wa chakula Haiti: WFP

El-Niño na ukame yahatarisha upatikanaji wa chakula Haiti: WFP

Uhaba wa chakula unakumba Haiti, wakati ambapo nchi hiyo inakabiliana na ukame kwa mwaka wa tatu mfululizo, ukame unaozidi kushika kasi kutokana na El-Niño, limesema leo shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP.

WFP imeeleza kwamba watu wapatao milioni 3.6 wanakumbwa na ukosefu wa chakula nchini humo, miongoni mwao milioni 1.5 kwa kiwango kikubwa.

Utafiti uliofanywa na WFP umeonyesha kwamba asilimia 70 ya mavuno yameharibika kwenye baadhi ya maeneo ya nchi, huku nusu ya raia wa nchi hiyo wakitegemea kilimo kuishi.

WFP imesema itaongeza misaada yake ili kufikia watu milioni moja waliokumbwa na ukame kwa kusambaza vifurushi vya vyakula na pesa.

Aidha imesema kwamba tayari imeshawasaidia watu 120,000 tangu mwezi Novemba na kuwapatia pesa watu 30,000 walioshiriki miradi ya kukarabati miundombinu.